Pages

Saturday, November 23, 2013

SUPER GLUE KWA KOPE....!!!!






AMA kweli hujafa hujaumbika, mrembo Khadija Omar, mkazi wa Kigogo, Dar amepata pigo kufuatia kupofuka macho alipokuwa akiwekwa nyusi bandia katika saluni moja iliyopo maeneo hayo, Risasi Jumamosi lina mkasa mzima.
Tukio hilo lilitokea Novemba 14, 2013 na kuvuta hisia za watu wengi waliosikia na kushuhudia mkasa huo.
Akizungumza na paparazi wetu juzi huku akimwaga machozi, Khadija alisema siku ya tukio saa 11 jioni alikwenda kwenye saluni hiyo iliyopo jirani na anapoishi kwa lengo la kubadili mwonekano wake wa macho kama akina dada wengine wanavyofanya.

“Mara tu baada ya kunibandika kope nilianza kuona giza, nikawaeleza akina dada waliniweka lakini wakanipuuza na kuniambia mimi ni mwoga.
“Muda mfupi mbele hali yangu ikawa mbaya zaidi, ikabidi wazibandue kope lakini juhudi zao ziligonga mwamba kwa sababu walitumia gundi kali, ikabidi nirudi nyumbani,”alisema Khadija.
Akaongeza: “Nikiwa njiani macho yaliniuma sana na kuzidi kupoteza uwezo wake wa kuona, ghafla nikaanguka chini. Akatokea msamaria mwema na kunipeleka nyumbani,” aliongeza.
Khadija alisema kesho yake alikimbizwa Hospitali ya Amana, Dar ambako alipatiwa dawa bila ya kutolewa kope hizo na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
“Nilipofika nyumbani hali ilizidi kuwa mbaya nikalazimika kupelekwa  Hospitali ya Macho ya CCBRT (Msasani, Dar) ili kupatiwa ufumbuzi wa tatizo hilo,” aliongeza Khadija kwa majonzi.
Alisema kule CCBRT alijikuta akiangua kilio baada ya madaktari kumwambia kope hizo haziwezi kutolewa mpaka zikatwe na mkasi.
Baada ya zoezi hilo kufanyika, Jumapili iliyopita Khadija aliweza kufungua macho kwa mara ya kwanza tangu alipotokewa na hali hiyo lakini bila kuona sawasawa.
Jumatatu iliyopita Khadija aliruhusiwa kurudi kwake lakini akiwa hana uwezo wa kuona na kutakiwa kurejea tena hospitalini hapo baada ya wiki tatu kwa uchunguzi zaidi.
Daktari mmoja wa CCBRT ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake gazetini alisema: “Khadija anaweza kuona kama zamani lakini itamchukua muda mrefu kutokana na madhara ya gundi ya ‘supa glu’ iliyotumika.
Taarifa zaidi zinasema, Jane na Koku wafanyakazi wa saluni waliomuweka kope hizo Khadija  walikamatwa na Polisi wa Kituo cha Magomeni jijini Dar na kufunguliwa jalada la uchunguzi namba MGN/RB/13021/2013.

No comments:

Post a Comment